Jumanne, 22 Aprili 2014 11:20

Je nitumie Joomla 2.5 au 3?

Written by
Rate this item
(0 votes)

Nimekuwa nikipokea email na hata simu toka kwa baadhi ya wateja wangu au watu mbalimbali ambao wamekuwa wakisoma makala au kuangalia mafundisho yangu.Moja ya swali ambalo limekuwa likijirudia ni kuwa, tayari Joomla 3 imeshatoka, je kwanini nisiende moja kwa moja hadi Joomla 3 badala ya 2.5? Ili kujibu swali hili kuna mambo kadhaa inabidi kuzingatia.

Toleo la mpito au toleo lililokamiilika?

Ili tuweze kufahamu lini ni muda sahihi wa kuhama au kutumia toleo husika la joomla ni vyema tukajua mtindo wa utoaji wa matoleo kwa joomla. Joomla wana utaratibu wa kutoa matoleo ya aina mbili, moja ni la mpito (Short Term Support - STS) na lingine ni lile lililokamilika au kwa lugha nyingine unaweza kusema lililokua (Long Term Support - LTS).

Kwa kawaida, toleo la mpito ni muhimu kwa ajili ya maandalizi kuelekea kwenye toleo lililokamilika, pia kwa kutumia matoleo haya ya mpito, Joomla huwawezesha watengenezaji wa viendelezo vya Joomla (Joomla Extensions) kujiandaa na kujua mfumo uliotumika kwenye utengenezaji wa toleo husika. Mtindo huu wa utoaji wa matoleo kwa Joomla unaweza kuufananisha na ule wa Microsoft kwenye mitambo endeshi yao, kwa mfano Windows Vista ilikuwa kama toleo la mpito kuelekea kwenye toleo lililokamilika ambalo ni Windows 7.

Kwa kawaida, kikomo cha matoleo ya mpito ni muda mfupi mno kulinganisha na yale yaliyokamilika, hivyo, mara nyingi watu hushauriwa kusubiri toleo lililokamolika pindi unapotengeneza wavuti yako ya kazi (siyo ya majaribio).

Ili kurahisisha na kutoa mwanga kwa watumiaji wake, Joomla hutoa mfumo (ratiba) ya utoaji wa matoleo yake, hivyo hii huwafanya watumiaji hao kuwa na taarifa ya kutosha juu ya matoleo ya Joomla.

Hivyo basi, kama unataka kutengeneza wavuti ya kazi (siyo ya majaribio), tunakushauri usubiri hadi pale toleo lililokamilika kama inavyooneshwa kwenye ratiba ya matoleo hapo chini.

Faida nyingine ya kusubiri hadi toleo lililokamilika ni kuwa, kwa kawaida, matoleo ya mpito hutumika kwa ajili ya uangalizi na kujaribu hivyo huwa na maboresho ya mara kwa mara, kwa kutumia matoleo haya, inakulazimu kufanya maboresho

kila mara yanapotoka kitu ambacho hutumia muda na kushindwa kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama wa wavuti yako.


Nini cha kuzingati?

Kitu cha muhimu kuzingatia ni kuwa, kuanzia Joomla 2.5, uboreshaji wa Wavuti iliyotengenezwa kwa Joomla toka toleo moja hadi lingine utakuwa ni rahisi mno, tofauti na ilivyokuwa kwenye Joomla1.5 kwenda 2.5 ambapo ulitakiwa kuhamisha
wavuti nzima.

Hitimisho:

Ingawa tunashauri sana kwa watumiaji wa Joomla kusubiri mpaka toleo lililokamilika ambalo ni Joomla 3.5, ila kama wewe ni kati ya wale wanaopenda kujaribu, una uzoefu wa kutosha kwenye Joomla, basi unaweza kuhama moja kwa moja hadi
Joomla 3.5 ukizingatia viendelezi vingi ambavyo vinafanya kazi kwenye Joomla 2.5 pia vitaweza kufanya kazi kwenye Joomla 3.5 bila tatizo lolote.

Je una swali juu ya makala hii au Joomla, tumamaoni hapa au unaweza kwenda kwenye Forum.

 

Hassan Ayeko

Hassan ni mtaalamu wa masuala ya IT pia ni mkalimani mkuu wa Joomla Kiswahili (Joomla Coordinator for Swahili language)

www.att-center.de